WATU WANNE MBARONI KWA KUMUOZESHA MWANAFUNZI WA DARASA LA TANO

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashilikilia watu wanne baada ya kuwanasa kwenye sherehe ya harusi wakimuozesha binti mwenye umri wa Miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano shule ya Msingi Samuye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambaye ametolewa mahari ya ng’ombe nane na shilingi laki sita (600,000/). Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Septemba 14,2020 majira ya saa kumi na mbili na dakika arobaini jioni, katika kijiji cha Isela, kata na tarafa ya Samuye, halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Kamanda Magiligimba amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Geni Bundala (52), Jumanne Shigimahi (54),Hawa Ramadhan (37) na Japhari Khalfan (52) wote ni wakazi wa kijiji cha Isela. Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka 12 aliozeshwa kwa kutolewa mahari ya ng’ombe 8 na pesa tasilimu laki sita za Kitanzania. Kamanda Magiligimba anatoa wito kwa wananchi hususani wazazi na walezi mkoani Shinyanga kuacha kuozesha wanafunzi kwani inapelekea watoto wa kike kukatisha ndoto zao za kuendelea na masomo na hivyo kupelekea kukosa viongozi wanawake wa baadae.

Comments